Wanafunzi wa Chuo cha Uuguzi cha Bulongwa kilichoko Wilaya ya Makete
mkoani Iringa, wamemuua kwa kumshambulia kichwani mkufunzi wa chuo
hicho, Dk. Jumbe Mafingo, kwa madai ya kupinga jaribio lake la kutaka
kumbaka mwanafunzi mwenzao.
Taarifa za awali za makachero wa polisi
zilieleza kuwa mkufunzi huyo aliuawa baada ya kutuhumiwa kwamba alitaka
kumdhalilisha kijinsia mwanafunzi wa kike, Jean Laison Mwakabuta kwa
kutaka kumbaka.
Tukio hilo la kuuawa kinyama kwa mkufunzi
huyo ambaye ni mwalimu wa nidhamu chuoni hapo, lilitokea juzi usiku
nyumbani kwake mjini hapa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Iringa, Evarist Mangalla, Dk. Mafingo alifikwa na umauti baada ya
mwanafunzi huyo kuamua kwenda nyumbani kwake usiku ili kumkabidhi
maelezo yake ya kimaandishi kuhusu sababu zilizomfanya alale nje ya
chuo.
Ilielezwa kuwa muda mfupi baada ya kuingia kwenye nyumba ya mwalimu huyo, mwanafunzi huyo alianza kupiga kelele kuwa anabakwa.
Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa Bwana Evarist Mangalla
Alisema kufuatia kelele hizo, wanachuo
wengine waliamka katika vyumba vyao na kwenda hadi eneo la tukio na
kuanza kumshambulia kichwani mkufunzi huyo hadi kumuua.
Kamanda Mangalla alisema Dk. Mafingo aliuawa kwa kushambuliwa na kitu kizito kichwani.
“Huyu Jean Laison Mwakabuta, aliambiwa na
Dk. Mafingo ambaye ni mwalimu wa nidhamu chuoni hapo, aandike maelezo
ya maandishi kwa sababu gani alilala nje ya chuo,...baada ya kuandika
maelezo hayo, aliamua kuyapeleka nyumbani kwa mkufunzi huyo usiku, sasa
baada ya kugonga mlango na hatimaye akaruhusiwa kuingia, alianza kupiga
kelele kwamba anabakwa…na ndipo wanafunzi wenzake waliposikia kelele
wakaamka na kukimbilia eneo hilo na kumshambulia mkufunzi huyo hadi
kufa,” alisema Kamanda Mangalla.
Ilidaiwa kuwa siku moja kabla ya tukio
hilo, uongozi wa chuo hicho cha Bulongwa ulitoa ridhaa kwa wanachuo wote
kwenda kutembea nje ya chuo kwa lengo la kuwapunguzia msongo wa mawazo
ya masomo na Jean Laison Mwakabuta hakurejea chuoni hadi siku
iliyofuata.
Kamanda Mangalla, alisema wanachuo wanne akiwamo mwanafunzi Jean, wametiwa mbaroni kuhusiana na mauaji hayo.
Chanzo: Nipashe
Comments