MLIPUKO WA BOMU ARUSHA
Charles James Kahela
Bwana Charles James Kahela, mkazi wa Arusha hadi sasa anaona kama ni muujiza kwake kubaki hai, kwani haamini na wala haelewi kwa nini yeye apone wengine wafe.
Akitoa ushuhuda wake kanisani, Bwana Charles alisema,
"Baada ya kutoka kazini niliamua kupitia kwenye mkutano wa Chadema ambao ndio ulikuwa unafikia mwisho na kwa sababu mahali pale palikuwa karibu sana na kwa bosi wangu, nikaamua ngoja nami nisipitwe niende kusikiliza chochote kutoka kwa mwenyekiti wa CHADEMA Taifa Bwana Freeman Mbowe." Alifuta machozi, kisha akaendelea.
"Wakati mkutano umefika mwisho na watu wakiondoa baadhi ya vitu uwanjani huku viongozi nao wakiowa wametoka jukwaani, nilisikia kitu kimerushwa nyuma yangu karibu kabisa na kichwa changu na kwenda kutua mbela ambako kulikuwa bado na watu wengi tu na watoto kadhaa. Nikasikia mlipuko mkubwa sana, baada ya muda nikaona watu wamelala chini na damu nyingi sana zikimwagika. Kweli ilikuwa ni hatari sana, sijawahi kuona tukio baya kama hilo. Muda si muda polisi waliwazingira viongozi wa Chadema kwa ajili ya ulinzi huku wengine wakianza kurusha risasi kuelekea upande wa wananchi waliokuwa wakitoa kipigo kwa mtu mmoja aliyedhaniwa kuonekana akirusha bomu. Ilikuwa ni hatari tupu. Ilinibidi kuvunja mojawapo ya mageti ya mbao ya nyumba jirani na kulala chini ili kukwepa risasi ambazo zilikuwa zilirushwa chini chini sana. Mpaka sasa hivi ninavyoongea bado mwilini mwangu nasikia joto sana na kutetemeka." Alimaliza Bwana Charles.
Kwa mujibu wa taarifa ya habari ya Redio One Stereo ya saa 2:00 usiku, serikali ilisema kwamba mlipuko uliotokea kwenye mkutano wa Chadema ilikuwa ni bomu la kutupwa kwa mkono. Waziri wa Mambo ya Ndani Dr Emmanuel Nchimbi aliyasema hayo wakati alipowatembelea waathirika wa bomu hilo katika hospitali za Mount Meru, St. Elizabeth na Serani zote za Jijini Arusha.
Nao uongozi wa mkoa wa Arusha umewaomba wananchi kuweka pembeni itikadi zao za kisiasa na kushirikiana kuwabaini watu waliohusika na milipuko wa bomu
Comments