Baada ya kusubiri miezi, wiki, siku na hata saa hadi dakika hatimaye wakati ulitimia pale ulipotokea mtanange mkali wa kukata na shoka kama sio mundu kati ya watani ama maadui wa jadi katika soka la bongo, Yanga na Simba, mchezo uliopigwa kwenye dimba la taifa huku ukitawaliwa na mbwembwe, fitina na majigambo toka kwa mashabiki wa pande zote mbili.
Mchezo ambao tumeshuhudia wana Jangwani Dar Young Africans wakiwazodoa watani wao alimaarufu wekundu wa msimbazi kwa kuwachapa magoli mawili moja katika kila kipindi cha mchezo huo.
Alikuwa ni Donald Ngoma aliyewainia mashabiki wa jangwani kwa kupachika bao baada ya kuunasa mpira uliopigwa na mabeki wa Simba wakirudisha pasi nyumba, ndipo akawalamba chenga beki na kipa wake na kuukwamisha wavuni.
Simba walijaribu kwa nguvu zote kurudi mchezoni na kufanikiwa kushambulia mara kadhaa lakini hadi kipindi cha kwanza kinaisha Yanga 1-0 Simba.
Kipindi cha pili nacho kilianza kwa kasi huku kila timu ikipanga mashambilizi lakini walionekana ni Yanga waliojipanga na ushindi leo baada ya Hamis Tambwe kuwainua wana Jangwani tena na kupachika goli safi sana katika dakika ya 27 kipindi cha pili.
Simba walijaribu kujitutumua ili angalao wapate hata goli la kufutia machozi au kusawazisha lakini siku haikuwa yao leo ukizingatia kwa muda mrefu wamecheza wakiwa pungugu baada ya mmoja wao kupewa kadi nyekundu.
Hivyo hadi mwisho wa mchezo huo uliowaweka kileleni Yanga kwa kufikisha alama 46, Yanga 2, Simba 0.
Comments