Skip to main content

Waziri Mstaafu Lazaro Nyalandu aendelea kutoa ya moyoni kwa jamii

BAADA ya kutenda mema, wakasema ASULUBIWE! Na LazaroNyalandu

NIMEINGIA Wizara ya Maliasili na Utalii kwa uteuzi wa Rais Jakaya Kikwete, Mnamo Februari 10, 2014, na nimefanya kazi ya Uwaziri kwa takribani miezi 18.

Itakubukwa kwamba kipindi hiki kilikuwa ni kilele cha ujangili wa Tembo barani Afrika, huku Tanzania ikitajwa kuwa nchi kinara kwa masuala ya ujangili wa wanyamapori, hususani Tembo. Wakati huo, akiba ya meno ya Tembo katika Ghala la Taifa yalifikia takribani tani 130,000, ikiwa ni idadi kubwa ya meno ya Tembo yaliyohifadhiwa popote duniani.

Kazi yangu ya kwanza ilikuwa ni kuongozana na Rais Jakaya Kikwete kwenda London, Uingereza kuhudhuria Mkutano wa Tembo duniani ulioandaliwa na Mwana Mfalme Charles wa Uingereza, ambako pamoja na mambo mengine, Rais Jakaya Kikwete aliitaarifu dunia juu ya uamuzi wa Tanzania wa kupiga marufuku biashara ya meno ya Tembo, na kuungana na Mataifa lukuki yaliyokubali kufanya hivyo.

Aidha, kwa kushirikiana na Rais Jakaya Kikwete, tulikubali Tanzania kujiunga na Mataifa 6 barani Afrika (African Elephants Range States), ikiwepo Ethiopia, Kenya, Gabon, Chad, Botswana na mataifa mengine kwa lengo la kuongoza mapambano hayo. Mara baada ya Mkutano wa London, Tanzania na baadhi ya Mataifa ya Afrika yalikuwa washiriki wa Pound milioni 10 zilizotolewa na UINGEREZA kupambana na uhalifu huo Afrika. Niliporejea Tanzania, nilianzisha Mpango wa Kuhifadhi Vema Akiba ya Meno ya Tembo nchini kwa kuyafanyia utambuzi wa DNA (asili, umri wa Tembo, na alikotokea) na kuhakikisha hayapotei, kazi iliyofanywa kwa ushirikiano kati ya watalaamu wa Wizara na Shirika la STOP IVORY UK.

Aidha, kama Waziri, kwa idhini ya Rais, nilihojiwa na Stephen Sucker wa kipindi maarufu Cha BBC HardTalk, nikiwa Mtanzania wa Pili wakati huo kuhojiwa HardTalk,  wa kwanza akiwa Rais Mstaafu Benjamin William MKAPA, na nilipata fursa ya kuielezea dunia azma ya Tanzania kuongoza mapambano dhidi ya Ujangili  barani Afrika.

Kwa kuzingatia changamoto waliyokuwa nayo wahifadhi kote nchini, niliiongoza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kufanya mchakato wa kuongeza idadi ya Maaskari wa Wanyamapori kutoka 1000 hadi 4000, na kuanzisha mazoezi mahsusi kwa Maaskari wa Wanyamapori katika Pori la Akiba la Selous kwa kushiriana wa kikosi Maalum Cha US Special Forces kilichopo mjini Stuttgart, Ujerumani. Maaskari wa Wanyamapori walifundishwa umahiri na weledi katika kufanya kazi yao, na walipatiwa, kwa kushirikiana na Serikali ya Marekani, vifaa vya kuwawezesha kumudu hali yenye changamoto wanapokuwa porini. Aidha, Serikali ya Ujerumani ilikubali kutoa Uniforms na boots kwa ajili ya Askari wetu, ikiwa ni hatua za awali za kuwajengea morali na utayari wa kuitumikia nchi wanapokuwa katika mazingira tete porini.

Wakati huo huo, Taasisi ya Howard Buffet Foundation ilikubali kutoa helikopta kwa ajili ya Doria, Shirika la FZS walitoa ndege yenye kamera maalumu (infra red), Friedkin Conservation walikubali kutoa helikopta, Kilimanjaro Safari Club walitoa ndege, na Mkuju River Project walitoa ndege. Ndege ya FZS ilikuwa na kamera maalumu (infra red) zinazoweza kuwatambua majangili porini nyakati za usiku. Taasisi ya HBF, ilitoa fedha, magari, pamoja na kukikarabati Chuo Cha Maaskari wa Wanyamapori Pansiasi Mwanza na kununua vitendea kazi vingine kwa ajili ya maaskari wanafunzi.

Tukiwa tumeongeza idadi ya wapiganaji, nilishirikiana na Taasisi ya Paul Allen (mwanzishi mwenza wa Microsoft) kuidadi (kuhesabu) upya Tembo nchi nzima, ambako baada ya mwaka moja, idadi ya Tembo ikaanza kuongezeka sana kutokana na jitihada hizi shirikishi. Aidha, kupitia Paul Allen, tulianzisha mfumo mpya wa mawasiliano Selous uitwao Digital VHS, wenye lengo la kuwawezesha Maaskari kuwa na mawasiliano yasiyoingiliwa kimtandao na majangili na watu wengine wenye nia mbaya.

Halikadhalika, kwa kuzingatia hali tete ya kupotea kwa Tembo katika hifadhi ya Ruaha wakati huo, nilishirikiana na Serikali ya Marekani kupitia Taasisi ya WCS (World Conservation Society) yenye Makao yake Makuu mjini New York, ambayo ilianzisha mradi wa muda mrefu wa dola milioni 50 kuokoa Hifadhi ya Ruaha pamoja na maeneo mengine.

Mwaka huo huo, kwa kushirikiana na Shirika la International Conservation Caucus (ICCF) la Mjini Washington, DC, pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa UNDP-Tanzania na Benki ya Dunia, (ofisi ya Tanzania) niliitisha Mkutano wa Nchi 11 za Africa uliofanyika mjiini Arusha, na kukubaliana juu ya Azimio la Arusha “Arusha Declaration” kuhusu kushirikiana kuhifadhi maeneo yanayoingilina (shares ecosystems) katika nchi zetu. Washiriki wa Maendeleo ikiwepo Ujerumani, UNDP, na Marekani walishiriki nami katika kutia sahihi makubaliano kati ya Tanzania na Msumbiji (Selous-Niassa Corridor Agreement) tuliyoyafikia mjini Maputo, Msumbiji kuhusu kulinda ushoroba wa Selous-Niassa kati ya Msumbiji na Tanzania unaokadiriwa kuwa na ukubwa wa  kilometa za mraba 40,000, ukiwa ni ushoroba mkubwa kuliko zote duniani.

Nilichukua hatua ya kuzishauri na kukubaliana na nchi zenye misitu ya asili ‘miombo woodland’ ambayo ndio misitu ya asili kwa Hifadhi ya Tembo barani Afrika zikubali kutia saini “Miombo Woodland Agreement”, ikiwa ni sehemu ya jitihada za mataifa haya kuhifadhi Tembo, na uoto wa asili wa Miombo, ambao unasaidia pia kuzuia mabadiliko ya tabia nchi duniani. Nchi zilizokubali ni pamoja na Zambia, Malawi, na Msumbiji, na tulianza hatua za awali za kufanya jitihadi za nchi hizi zijulikane na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa Wakati wa Mkutano wa Mabadiliko ya Tabia Nchi, Paris, Ufaransa. Tanzania na Zambia zilikuwa nchi za kwanza kuweka sahihi Makubaliano hayo.

Nilianza mchakato na Benki ya Dunia wa kutoa dola 150, 000,000  kwa ajili ya kusaidia kuinua Utalii kusini mwa Tanzania (mikoa ya kusini mwa reli ya kati), pia tulipata Euro milioni 50 kutoka Ujerumani kwa ajili ya kusaidia Uhifadhi kupitia uanzishwaji wa TAWA, na Serikali ya China ilitoa magari mapya na pikipiki maalumu za matairi matatu kwa gharama ya zaidi ya dola milioni Moja na nusu.

Aidha, kwa ushirikiano Mkubwa na wenzangu Wizarani, Nilifanikisha kuanzisha Taasisi Mpya kabisa Tanzania ya TAWA (Tanzania Wildlife Authority), inayochukua kazi za kiuhifadhi za idara ya Wanyamapori. Nilishirikiana na wenzangu Wizarani kuandaa mfumo wa uendeshaji wa taasisi hii ili iweze kuwa kinara Cha Uhifadhi nchini kwa kumiliki na kulinda mapori yote ya Akina (Game Reserves), Mapori Tengefu, na maeneo yote ya Wanyamapori yaliyo NJE ya uangalizi wa Tanapa  au Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Serikali ya Ujerumani, kama nilivyosema hapo awali, ilitoa Euro milioni 50, na Serikali ya Tanzania ilikubali Shirika hili la Umma liwe na Makao yake Makuu Mjini Morogoro.

Baada ya kuleta helikopta Wizarani, nilianzisha mpango maalumu wa kuwafundisha vijana wa Kitanzania mafunzo ya urubani wa Helikopta na ndege nchini Afrika Kusini na Marekani, na tayari kuna vijana waliofuzu vema.

Pamoja na kwamba siwezi kuyaeleza yote kwa sasa, ikumbukwe kuwa nilianzisha Tangazo la “Tanzania, the Soul of Africa”, nilianzisha Swahili Expo kwa ushirikiano na Indaba SA, na tulifanikiwa kwa ushirikiano na wadau wa Utalii nchini, kuongeza idadi ya watalii kuvuka milioni na pato la Utalii kufikia dola bilioni 1.3, huku Benki Kuu Tanzania ikiarifu kuwa Sekta ya Utalii wakati huo ilikuwa inaongoza kwa kuingiza nchini Fedha za kigeni, forex.

HIZI ni baadhi ya KAZI nilizozifanya ndani ya miezi 18 nilipokuwa Waziri wa Maliasili na Utalii.

Waziri Kigwangalla pamoja na wale waliopania kuniumiza wanahitaji miwani yenye lensi za ziada yamkini kwamba, macho yao yaweze kuona, na ndimi zao ziweze kukiri mema haya ambayo MUNGU alitujalia kuyafanya kwa pamoja nikiwa Waziri wa Maliasili. Iliandikwa zamani, “Kama hamniamini mimi, basi aminini kazi ninazozifanya”. Miaka zaidi ya miwili baada ya mimi kumaliza kazi yangu ya uwaziri nikiwa salama, na baada ya kuhama CCM, wamenigeuza adui. Katika Wizara ya Maliasili, Mimi Nyalandu sikuwahi kufukuzwa, kuachishwa, wala kutumbuliwa muda WOTE nikiwa Wizarani, ikiwa ni historia kubwa ikizingatiwa kuwa Mawaziri wengi hawakumaliza Salama. Mwenye masikio na ayasikie maneno haya. MUNGU awakemee wote wanaokaa vikao vya SIRI kupanga hila juu yangu, MUNGU akalikomboe Taifa letu dhidi ya roho ya HOFU inayofanya wengi kunyamaza huku wakiona Taifa linaangamia, ikawe HERI kwa wote waitamanio HAKI, na ni maombi yangu kwamba MUNGU afufue UJASIRI, na afufue KAZI yake katikati ya MIAKA. Taifa Tanzania na watu wake watasimama TENA. Tushikane MIKONO. Tuamini. Tuungane.

SIGNED
Lazaro S. Nyalandu.
Waziri Mstaafu, Maliasili na Utalii, Tanzania

Comments

Popular posts from this blog

MAKUNDI CHAMPIONS LEAGUE NA SHIRIKISHO AFRIKA

Yanga Sc kundi A Klabu Bingwa Afrika na Simba Sc kundi A Shirikisho Afrika. Hapo chini ndio mpangilio wa makundi na timu zake. Je, nani kati ya timu zetu za bongo atatoboa kwenda robo fainali? Weka maoni yako kwenye komenti tafadhali.

Hawa Ndiyo Real Madrid Waliowafunga Man City Champions League Jana Usiku

Man City wakiwa wanaongo za kwa 2-1 dhidi ya Real Madrid huku zikiwa zimebaki dakika si zaidi  ya tatu walionekana kama ingekuwa ni timu ya tatu ya Uingereza kuifunga Madrid kwenye uwanja wa Bernabeu. Lakini vijana hao wa Mancini badala ya kuinza kampeni yao kwa ushindi walijikuta wakiachwa nyuma na kuwaangalia Madrid wakiibuka na ushindi baada ya Karim Benzema kusawazisha na kisha Cristiano Ronaldo kufunga goli la tatu na la ushindi, goli lililomfanya bosi wao Jose Mourinho kuslide uwanjani akishangilia goli hilo na Ronaldo. This was the real happiness now from Ronaldo BBC football pundit Robbie Savage alikuwa uwanjani huku Bernabeu. (quoting from BBC SPORTS) "Maicon was not at the races at all in the first half at right-back. He was a passenger and it was like City were playing with 10 men. Cristiano Ronaldo kept coming inside him. "In the second-half, Vincent Kompany looked at what was happening and came across to that wing more. Ronaldo did not...