Simu yake iliita kwa sauti msikitini wakati wa swala, ilikuwa bahati mbaya.
Imama alitoa khutba fupi ya mawaidha baada ya swala akimwelezea jamaa huyo kama mfano wa waumini wazembe.
Waumini wengine walimlaumu baada ya swala kwa kuwasababishia usumbufu katika swala zao.
Mkewe naye hakubaki nyuma, wakati wakirudi nyumbani aliendelea kumpa maneno kuhusu uzembe wake mpaka wanaingia nyumbani.
Ndugu wengine walitikisa vichwa vyao kuonesha kukerwa sana na jambo alilolifanya.
Alionekana kufedheheka, kuaibika na kudhalilika sana. Hilo lilijionesha usoni mwake.
Hakukanyaga tena msikitini.
Jioni ile alielekea Baa.
Alionekana mwenye mhemko na kutetemeka.
Alimwaga kinywaji chake mezani, chupa ilidondoka kwa bahati mbaya na kuwamwagikia baadhi ya watu.
Wale waliomwagikiwa na kinywaji chake walimkimbilia. Alifumba macho akitrajia kuzabwa vibao au kuambiwa maneno makali.
Badala yake walimuuliza kama ameumizwa na kipande cha chupa iliyovunjika.
Mhudumu alimpa pole na kumpa tishu ajisafishe.
Mfanyakazi wa usafi alisafisha sakafu.
Meneji wa kike alimpa kinywaji kingine kufidia kinywaji chake. Pia alimkumbatia na kumpiga busu shavuni huku akimwambia: "Usihofu. Kila mtu hufanya makosa".
Tangu wakati huo hajaacha kwenda baa.
#FUNZO
Wakati mwingine tabia zetu kama waumini huwakimbiza watu wazuri na kuwasukumia motoni. Tunadhani kuwa tunajua kila kitu. Tunadhani kuwa tuna hakika mia kwa mia kuwa tutaingia Peponi.
Unaweza kubadilisha hali ya mambo kutokana na unavyoamiliana na watu, hasa pale wanapofanya makosa.
* Kama huwezi kuwa daraja la kuunganisha watu, basi usiwe ukuta wa kuwatenganisha.
*Kama huwezi kuwa taa ya kuyaangazia mema ya watu, basi usiwe giza la kuzifunika juhudi zao.
* Kama huwezi kuwa maji yanayosaidia kustawisha mazao ya watu, basi usiwe mdudu anayeharibu mazao yao.
* Kama huwezi kuwa chanjo ya uhai, basi usigeuke kuwa virusi vya kukatisha uhai.
* Kama huwezi kuwa penseli ya kuandikia furaha ya mtu, basi jaribu kuwa ufutio mzuri wa kuondosha huzuni yake.
Daima tunaweza kuwa walinzi kwa wenzetu, tuwe na azma ya kuiponya dunia na kuifanya kuwa sehemu bora. Naam, tunaweza.
#UPENDO NI DARAJA KATI YAKO NA KILA KITU.
Imetafsiriwa na Maalim Ibrahim Kabuga.
#MoyoFoundation #Upendo #UislamuNiUpendo
Comments