Simba sc waingiza sh milioni 130 kila mwezi kutoka kwa mwekezaji wao Mo Dewji
OFISA Habari wa Simba, Haji Sunday Manara amesema kuwa Simba inaingiza fedha zaidi ya Sh milioni 130 kila mwezi kama gawiwo kutoka kwenye fedha ya mwekezaji.
Fedha inayotakiwa kutolewa na mwekezaji ni Sh bilioni 20 ili amiliki sehemu ya 49% ya klabu hiyo na Manara amesema fedha hizo kama walivyokubaliana zimeingizwa benki ambako watakuwa wakipata gawio ambalo tayari wameanza kulipata kwa kuchukua zaidi ya sh milioni 130 kila mwezi.
“Simba ishaanza kupokea sehemu ya gawio au ziada lakini kuna fedha tunapata kutoka katika fixed account. Mfano ukiweka milioni 100 kuna kiasi fulani unapata, sasa kwa fedha iliyowekwa sisi tunapata na inatusaidia katika masuala ya mishahara.
“Sisi niseme nia ya mabadiliko ipo na kubwa sasa Simba inakula fedha ya gawio kutoka katika fedha tuliyokubaliana iwekwe kama sehemu ya manunuzi ya Simba,” anasema Manara.
“Nimesikia hili limeibuliwa na haya ndiyo majibu yake na huenda wengi hawajui kwa kuwa hatujasema. Tunapata fedha hizi nyingi na kwa mwaka kupitia gawio hilo tunaweza kupata angalau Sh bilioni 1.5.
“Nilimsikia kiongozi mmoja anasema bajeti ya mwaka ni Sh bilioni 5 au 6 hivi, ndio maana nasema hii yetu haitoshi, ndio maana tunaendelea kujiboresha kwa lengo la kutunisha mfuko na kuifanya klabu iweze kujiendesha kwa uhakika.
“Angalia tunafanya na Equity Bank kwa lengo hilohilo, ile kadi moja ya mwanachama inauzwa Sh 22,000. Hapo Simba inapata Sh 14,000 na hapa lengo ni kutunisha mfuko utakaoweza kujiendesha lakini hata kununua wachezaji hao wakubwa.
@#saidgadsonsaid
Comments