WAGONJWA 37 WAPONA CORONA, 71 WASUBIRI VIPIMO VYA MWISHO
Wagonjwa 37 waliokuwa wameambukizwa virusi vya Corona #COVID19 wamepona na kuruhusiwa kurejea nyumbani baada ya vipimo vya mwisho kuthibitisha kwamba hawana maambukizi.
“Watu hawa 108 hawana dalili zozote za ugonjwa kama vile homa au mwili kuchoka isipokuwa wapo katika vituo vya matibabu kusubiri vipimo vya mwisho ili kuthibika kwamba hawana virusi vya corona kabla ya kuruhusiwa kutoka vituoni,” amesema Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy Mwalimu amewataka watu waliopona ugonjwa huo kuzingatia maelekezo ya wataalamu wa afya ili kujikinga na maambukizi mapya ya COVID-19 kwani zipo tafiti zilizofanyika nchi mbalimbali ikiwamo China zimeonyesha kuwa watu wanaweza kupata maambukizi mapya kama asilimia 14.
“Tunapenda kuwahimiza watu waliopona watoe elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya Corona (COVID-19) kwa jamii. Pia, Nitumie fursa hii kwa niaba ya Serikali kutoa shukrani zetu za thati kwa watumishi wa afya kwa kuendelea kutoa huduma kwa watu wenye maambukizi ya COVID-19. Asanteni sana watumishi wa afya,” amesema Waziri Ummy.
Waziri pia ametoa wito kwa watumishi wa afya kuendelea kutoa huduma za afya kwa watu wote wanaohitaji huduma za matibabu wakiwamo wenye dalili za ugonjwa wa Corona.
“Tumeona kumeanza tabia ambayo ni kinyume na taratibu za afya, hatutakiwi kuwakataa wagonjwa wenye dalili za maambukizi ya virusi vya Corona,” amesema Waziri Ummy.
Wakati huo Waziri Ummy Mwalimu ameishukuru kampuni ya Azam group kwa msaada wa sabuni 300 na fedha shilingi milioni 50 kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Msaada huo utatumika kwa chakula cha wagonjwa na usafi kwenye vituo vya tiba cha Temeke,Amana na Kisoka-Mloganzila
#AzamTv
#BongoOnlineNews
#Covid19 ni hatari. Jikinge. #Kinga ni bora kuliko #tiba
Comments